Ujenzi wa barabara ya juu (flyover) unaoendelea katika makutano ya Barabara ya Nelson Mandela na Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam unatarajia kukamilika kabla ya muda uliokuwa umekadiriwa.
Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 100 unaojengwa kwa msaada wa serikali ya Japan umefikia asilimia 74.68 ya ukamilifu wake.
Mhandisi wa mradi huo kutoka Tanroads, Rajab Manger jana aliueleza ugeni kutoka Lesotho kuwa mradi huo ulipaswa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu lakini inaonekana utakamilika kabla ya muda huo.
“Kwa kiwango hiki, mradi unaweza kukamilika kabla ya mwezi Oktoba. Tuko mbele ya ratiba. Nina uhakika kwamba waendesha magari na pikipiki hivi punde wataanza kuondokana na tatizo la msongamano wa magari,” alisema Manger.
Aliongeza kuwa wahandisi wa mradi huo wameendelea kufanya kazi nzuri na kwamba hakuna ajali kubwa ambayo imetokea tangu kuanza kwa ujenzi huo mwaka 2016.