Mkaazi wa Hai mkoani Kilimanjaro, Irene Shao amedai kupewa adhabu ya kudeki ofisi ya Mtendaji wa kata kwa muda wa miezi mitatu akidaiwa kukaidi agizo la kufanya usafi mwisho wa mwezi.
Shao ambaye ni muuza magazeti katika eneo hilo, ameeleza kuwa alirejea kutoka mjini kufuata magazeti siku ya Alhamisi ya mwisho wa mwezi na ndipo alipokutana na adhabu hiyo baada ya kudaiwa kukaidi maelekezo.
Alidai kuwa yeye alikuwa akifahamu siku ya usafi ni Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwamba hakuwa anafahamu kama kulikuwa na mabadiliko katika kata hiyo ya kufanya usafi kila Alhamisi ya mwisho wa mwezi.
“Sikuwa na taarifa ya mabadiliko ya siku ya usafi. Kwahiyo siku ya Alhamisi niliendelea na majukumu yangu ya kila siku kufuata magazeti mjini hivyo nilikuta tayari usafi umeshafanyika. Mtendaji alisema nimekaidi, akanipa adhabu ya kudeki ofisi yake kwa miezi mitatu,” Shao anakaririwa na Mwananchi.
Shao alishindwa kuanza kuitumikia adhabu yake siku iliyofuata, hivyo hofu ya kuathibiwa tena ilimsumbua.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Hai, Edward Ntakilino alisema kuwa siku ya usafi ni Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwamba adhabu ya aliyekaidi ni faini ya shilingi 50,000 au kufungungwa jela mwaka mmoja.
Maagizo hayo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasssan katika hatua za kutunza mazingira na kuwa nchi safi inayoepuka magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira.