Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameachiwa huru kwa dhamana ya Polisi yenye thamani ya Milioni 50 muda huu baada ya kulala mahabusu kwa usiku mmoja.
Zitto alikamatwa na Jeshi la polisi siku ya jana, Alhamisi kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali maalumu.
Kamanda wa Polisi Morogoro, Ulrich Matei alidai kuwa walimshikilia kiongozi huyo kwa mahojiano na awaeleze alitoa wapi kibali cha kufanya mikutano ya chama katika maeneo ya nje pamoja na kujua kitu alichokua akizungumza na wananchi wa kata ya kikeo wilayani Mvomero.
Aidha taarifa za Zitto kuachiwa huru zimetolewa na Wakili wake, Emmanuel Lazarus Mvula ambae ndie aliyemdhamini Zitto na kusema anatakiwa kuripoti katika kituo kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Morogoro siku ya Jumatatu Machi 12, 2018.
Mbunge Zitto Kabwe alikamatwa na Jeshi la Polisi la Mkoa wa Morogoro wakati akiwa katika muendelezo wa ziara yake iliyoanza Februari 19 akiwa pamoja na viongozi wengine wa ACT- Wazalendo wa malengo ya kushiriki kazi za maendeleo na kuzungumza na kamati za maendeleo za kata hizo.