Watu wanaolima zao haramu la bangi wamebadili mbinu na kuhamishia kilimo chao katikati ya misitu baada ya mbinu za awali kubainika na kunaswa na jeshi la polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo ambaye alikuwa kwenye oparesheni iliyoongozwa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba katika eneo hilo amesema kuwa jeshi hilo limebaini mbinu mpya inayotumika katika eneo la msitu ulio karibu na Mlima Meru.
“Tunajua mbinu wanazotumika sasa hivi hapa Arusha na hatutarudi nyuma katika jitihada zetu za kupambana na kilimo cha bangi ambacho kinaharibu vijana wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa jeshi hilo halitamuonea huruma yeyote anajihusisha na kilimo au biashara ya bangi.
Katika oparesheni hiyo, walifanikiwa kuchoma moto hekari sita za mmea huo ambao matumizi yake ni kinyume cha sheria za nchi.
- Maelfu waandamana kupinga uamuzi wa Israel dhidi ya Waafrika
- Viongozi Kenya watofautiana kauli kuhusu Utalii Tanzania
Awali, wakulima wa zao hilo walikuwa wakilificha katikati ya mazao mengine ya chakula, mbinu ambayo ilibainika na kufyekwa.
Hivi karibuni, magunia ya bangi iliyotayarishwa kwa ajili ya matumizi yalikamatwa na jeshi hilo yakiwa yanasafirishwa kwa ajili ya kuuzwa mkoani humo na Dar es Salaam. Mengine yalikamatwa yakiwa yanaelekea nchi ya jirani ya Kenya.