Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli atafahamu hatma ya kesi yake kesho ambapo hukumu inatarajiwa kusomwa.
Sugu ambaye anashtakiwa pamoja na Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Nyanda za Juu, Emmanuel Masonga, anadaiwa kuvunja sheria kwa kutoa matamshi hayo Disemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika jijini humo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya inatarajiwa kutoa uamuzi wake kesho baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.
Upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa sauti zinazodaiwa kuwa ni za washtakiwa wakiwa wanatenda kosa hilo. Washtakiwa walikana kutoa maneno yaliyotajwa dhidi ya Rais Magufuli.
Sugu na Masonga wanawakilishwa na wakili Peter Kibatala ambaye alichukua nafasi ya kuwatetea baada ya mawakili wa awali, Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hakima Mwasipu kujiondoa kwenye kesi hiyo.