Uongozi wa klabu ya Young Africans umekanusha vikali tetesi kuwa nyota wao Obrey Chirwa atajiunga na watani wao Simba baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Raia huyo wa Zambia amehusishwa kutaka kujiunga na Simba kufuatia wiki iliyopita kocha msaidizi wa Wekundu hao Masoud Djuma kumwagia sifa mshambuliji huyo.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, Hussein Nyika amesisitiza kuwa mshambuliaji huyo ataendelea kusalia na mabingwa hao na kuhusu kujiunga na Simba alisema jambo hilo halitatokea kamwe.
“Kuhusu Chirwa kujiunga na Simba hilo suala halipo na halitatokea, Chirwa ni mchezaji wetu na hataenda popote tutamalizana nae na ataendelea kubaki hapa,” alisema Nyika kwa kujiamini.
Hata hivyo mkataba wa Chirwa na mabingwa hao utamalizika mwishoni mwa msimu huu hivyo mabingwa hao wanatakiwa kupambana ili kufanikisha jambo hilo.
Chirwa ndiye kinara wa ufungaji kwa mabingwa hao mpaka sasa akifunga mabao 11 manne nyuma ya kinara Emmanuel Okwi.