Serikali imepeleka shilingi bilioni 1.92 katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wilayani Mtwara kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya na kuwasisitizia watendaji kutobadilisha matumizi ya fedha hizo pindi wazipatapo.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa Halmashauri hiyo, wakati wa ziara ya kikazi mkoani Mtwara, ambapo amesema kuwa fedha hizo zimetolewa na serikali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Amesema kuwa ujenzi huo utahusisha chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume, eneo la kuchomea taka na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao,”amesema Majaliwa
Aidha, Majaliwa amewataka wananchi hao kuendelea kuiunga mkono serikali yao ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.
Hata hivyo, Majaliwa amesema serikali inatarajia kuipitia upya sheria ya elimu pamoja na sheria ya mtoto ili kuweka masharti ya kumlinda mtoto wa kike hususani kudhibiti mimba kwa wanafunzi.