Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa meli mbili zilizoonekana zikipeperusha bendera ya Tanzania kuelekea Korea Kaskazini zilishafutiwa usajili wake miaka miwili iliyopita.
Meli hizo zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Tanzania zilionekana kwa njia ya satelaiti, moja ikielekea Korea ya Kaskazini moja kwa moja na nyingine ilinaswa ikihamisha mizigo ambayo haikutambulika kwenye meli nyingine ambayo baada ya zoezi hilo la uhamishaji ilielekea Korea ya Kaskazini baada ya kupakia mizigo hiyo.
Waziri Mahiga amewaomba Mabalozi 6 ambao ni wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa Urusi na China kuisadia Tanzania kuweza kuzibaini meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania na kwenda kinyume na utaratibu wa kimataifa wa usafirishaji baharini.
Aidha, Januari mwaka huu serikali ya Tanzania ilizifutia usajili meli 450 zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kupatikana kwa meli iliyokuwa imebeba shehena ya silaha na dawa za kulevya huku ikipeperusha bendera ya Tanzania.
Hata ivyo, wiki moja iliyopita Rais wa Marekani, Donald Trump alitishia kuyawekea vikwazo vya Kiuchumi, Kidplomasia, Kisiasa na kibiashara mataifa yote yatakayokiuka vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa na Marekani dhidi ya Korea ya Kaskazini.