Katibu mkuu wa klabu ya Yanga, Boniface Mkwasa amesema mabingwa hao wanawatakia kheri watani wao Simba katika mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry kutoka Misri.
Simba itawakaribisha Waarabu hao keshokutwa Jumatano katika uwanja wa Taifa ambapo mchezo huo utaanza saa 12 jioni.
Mkwasa aliyasema hayo wakati akizungumzia maandalizi ya mchezo wao wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana utakaipigwa kesho saa 10 jioni katika uwanja huo huo wa Taifa.
Mkwasa alisema Simba inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Shirikisho Afrika kwahiyo itapendeza zaidi kama wataibuka na ushindi mbele ya Masry.
“Tunaitakia kheri Simba katika mchezo wake dhidi ya Al Masry keshokutwa, itakuwa vizuri kama watatoka na ushindi,” alisema Mkwasa.
Wakati huo huo Mkwasa amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kesho kuipa sapoti timu katika mechi hiyo ambayo wanahitaji ushindi.