Kikosi cha Azam FC kilichokuwa kwenye mapumziko ya siku nne, jana kimeanza rasmi mazoezi tayari kuivutia kasi Mtibwa Sugar, katika mchezo wa robo fainali, ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini, utafanyika Machi 31 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salam saa 1.00 usiku.
Taarifa iliyotolewa na afisa habari wa Azam FC Jaffar Idd Maganga, imeeleza kuwa, klabu hiyo imejizatiti kutinga nusu fainali kwa kuichapa Mtibwa ikiwa ni katika kutimiza malengo ya kulitwaa taji hilo.
Mshindi wa mchezo huo, ataenda kucheza ugenini na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya Stand United na Njombe Mji, watakaocheza Machi 30 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga saa 10.00 jioni.
Mbali na mechi hizo, Machi 31 Tanzania Prisons itawakaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni, huku Aprili Mosi hatua ya robo fainali ikimalizika kwa Singida United kukipiga na Yanga Uwanja wa Namfua, Singida saa 10.00 jioni.
Mbali na bingwa wa michuano hiyo kubeba kombe, medali na kitita cha shilingi milioni 50, pia atakata tiketi ya kuliwakilisha Taifa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.