Klabu ya Singida United imekanusha taarifa zilizo sambaa kuhusu kufungiwa miezi sita kwa mchezaji wao Daniel Lyanga na shirikisho la soka ulimwenguni (FIFA), Kwa madai kuwa mchezaji huyo alisaini na timu hiyo wakati bado akiwa na mkataba wa miaka miwili na klabu ya Fanja Fc ya Oman.
Klabu ya Singida United imetoa maelezo hayo kupitia ukurasa wake wa instagram, imesema ilifuata taratibu zote za usajili wa mchezaji huyo, usajili ulioshirikisha pande zote mbili kati ya Fanja Fc na Singida United ikiwemo kulipa fidia za gharama ya mkataba wake ulio kuwa umebakia na timu hiyo.
‘‘Kilichotokea ni kwamba ICT ya Daniel Lyanga ilichelewa kuja kutokana na dirisha la usajili kufungwa. Hivyo FIFA walituandikia barua sisi pamoja na TFF kwamba ICT ya Daniel Lyanga itakamilika hadi hapo dirisha kubwa la usajili litakapofunguliwa hapa Tanzania Kuanzia July 2018” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Mchezaji huyo hajaonekana uwanjani kuicheza singida United kwenye ligi kuu Tanzania bara kitendo kilicho zua maswali miongoni mwa wanamichezo na mashabiki wa soka hapa nchini.