Kampuni ya Facebook imeeleza kuwa sakata la kudukuliwa kwa taarifa za siri za watumiaji wa mtandao wake wa kijamii limewaathiri watumiaji zaidi ya milioni 87, tofauti na ilivyoelezwa awali kuwa ni watumiaji milioni 50.
Watumiaji wa mtandao huo walikumbwa na kadhia hiyo bila kujua hadi pale msamalia mwema, Christopher Wylie alipofichua kuwa taasisi ya kisiasa ya Cambridge (Cambridge Analytica) ilifanya udukuzi huo.
Muasisi wa Facebook, Mark Zuckerberg amekiri ongezeko hilo la waliodukuliwa akieleza kuwa kampuni yake ina wajibu na imejifunza kuwajibika zaidi kwa taarifa za watumiaji wake.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Zuckerberg alisema kuwa hivi sasa kampuni yake mbali na kuwapa watu nyenzo za kutumia itaendelea kuwajibika pia kwa kuamua namna ya kutumia nyenzo hizo.
“Leo tumeweza kufahamu… tunapaswa kuchukua hatua zaidi ya nyenzo tunazowapa watumiaji wa Facebook. Kwamba, hatutengenezi tu nyenzo, lakini pia tunatakiwa kuwajibika zaidi kwa matokeo ya matumizi ya nyenzo hizo,” alisema.
Wakaguzi wa ndani wa kampuni hiyo walibaini kuwa taarifa za watumiaji zimekuwa zikiingiliwa na kuchakachuliwa na baadhi ya watumiaji wenzao.