Majambazi wamevamia na kuvunja kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Mbezi Mwisho jijini Dar es salaam na kuiba pesa na vitu vya thamani vilivyokuwa kanisani humo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam, Lazaro Mambosasa, amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, ambapo majambazi hao waliingia kanisani humo na kuiba vitu ikiwemo fedha za sadaka zilizokusanywa tangu sikukuu za pasaka mpaka sasa.
“Ni kweli nimepokea simu kuwa kuna hilo tukio, ni vibaka wameingia hapo kanisani na kuiba pesa na baadhi ya vitu, pesa ambazo zilikuwa za sadaka tangu sikukuu, ila thamani yake bado hatujaijua kwa sababu ndio tukio limeripotiwa sasa, baada ya muda nitakuwa na taarifa kamili”, amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kuwabaini waliohusika na tukio hilo, ili kuwafikisha mbele ya sheria.