Kamati ya rufaa ya maadili ya shirikiso la soka nchini, TFF imetupilia mbali rufaa ya Michael Wambura aliyekuwa makamu wa Rais wa shirikisho hilo ambaye alifungiwa maisha kujihusisha na shughuli za soka.
Baada ya kupitia hoja zake za rufaa, kamati ya rufaa ya maadili imejiridhisha na maamuzi ya awali yaliyotolewa na kamati ya maadili kumfungia maisha Michael Wambura.
Kamati ya rufaa yamaadili imeiagiza TFF kulifikisha suala la Wambura kwenye vyombo vya sheria.
Wambura alipewa hukumu hiyo kufuatia kupatikana na hatia ya makosa matatu ikiwemo Kupokea fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013, Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013, kosa la tatu ni Kufanya vitendo vinavyoshusha Hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)