Majogoo wa jiji Liverpool, wamesema hawatoharakisha kumrejesha uwanjani mshambuliaji wao kutoka nchini Misri Mohamed Salah, na badala yake watamuacha apone kabisa majereha aliyoyapata wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Man City.
Meneja wa Liverpool Juergen Klopp, amewaabia waandishi wa habari kwenye mkutano uliokua na lengo la kuzungumzia mchezo wa kesho dhidi Everton, kwa kusema Salah hatokuwa sehemu ya kikosi chake.
Salah alipata majeraha ya nyonga na kulazimika kutolewa nje wakati wa mchezo dhidi ya Man City siku ya jumatano, ambao ulimalizika kwa wajogoo wa jiji kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
Klopp amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 bado anaendelea kupatiwa matibabu na huenda akachukua muda wa siku kadhaa kabla ya kurejea tena uwanjani kujumuika na wenzake.
“Sitaki kuharakisha kumtumia, ninajua umuhimu wake katika mchezo mgumu kama wa kesho, lakini sina budi kufuata ushauri wa madaktari na kumpa muda wa kupona kabisa,” Amesema Klopp.
“Sidhani kama italeta maana endapo nitamtumia katika mchezo wa kesho, hakuna mtu atakaependezwa na hilo, japo mashabiki wengi wanahitaji kumuona akicheza dhidi ya mahasimu wetu wakubwa Everton.
Salah, ambaye tayari ameshafunga mabao 38 katika michezo yote aliyoichezea Liverpool msimu huu, huenda nafasi yake hiyo kesho ikachukuliwa na Danny Ings, ambaye hajawahi kutumika tangu msimu huu ulipoanza.