Wakata miwa kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro Mtibwa Sugar, wameng’ara katika mchezo wao dhidi ya Singida Utd uliochezwa leo jioni katika uwanja wa Namfua mjini Singida.
Mtibwa Sugar ambao walifunga safari kutoka wilayani Mvomero mkoani Morogoro hadi mjini humo kwa ajili ya mchezo huo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, wamefanikiwa kuvuna point tatu muhimu na mabao matatu dhidi ya wenyeji wao.
Shughuli ya ushindi huo mkubwa kwa Mtibwa Sugar ilikamilishwa kupitia kwa Kelvin Sabato, Salum Kihimbwa na Hassan Dilunga.
Sabato alifunga bao la kwanza dakika ya 21 kwa shuti la mpira wa adhabu lililotinga nyavuni moja kwa moja, kabla ya Khimbwa kufunga bao la pili dakika ya 53 akimalizia pasi nzuri ya Dilunga, ambaye naye alifunga bao la tatu dakika ya 71 kwa penati.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki Roland Msonjo wa Singida United ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm, kumchezea rafu kiungo Salum Kihimbwa kwenye eneo la hatari.
Ushindi huo unaifanya Mtibwa Sugar kufikishe alama 30 baada ya kucheza michezo 21 na kuendelea kukamata nafasi ya sita, nyuma ya Singida United yenye pointi 36 kufuatia kucheza mechi 33.