Askofu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe leo hii anatakiwa kuripoti ofisi za uhamiaji kwa mahojiano na idara hiyo iliyopo jijini Dar es salaam baada ya kuandikiwa barua ya wito huo Aprili 5, mwaka huu.
Ambapo barua hiyo imemtaka leo hii saa 4:00 asubuhi awe tayari amekwisha ripoti katika idara ya uhamiaji.
Kufuatia agizo hilo amesema kuwa hawezi kutishika kwa kitu chochote kwani yeye sio unyasi na amewaomba waumini wake wasiyumbishwe na changamoto zinazojitokeza katika maisha kwani anaamini kuwa changamoto hizo zina lengo la kuharibu mahusiano yake na Mungu.
Kakobe alizungumza hayo jana pindi akifanya mahubiri katika ibada aliyoiendesha katika kanisa lake lilipo Mwenge jijini Dar es salaam.
Aidha, mbali na kuitwa Uhamiaji Kakobe amepitia misukosuko mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kumchunguza juu ya uhalali wa utajiri wake, na akaunti zake na watoto wake na kubainika kuwa fedha zote zilizoonekana benki ni mali ya kanisa, kwani ni fedha zinazotokana na sadaka, zaka pamoja na michango ya kanisa.