Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger amesema mpango wa kutangaza kung’atuka klabuni hapo, haukuwa sehemu ya malengo yake katika kipindi hiki, baada ya kuitumikia The Gunners kwa miaka 22.
Wenger amefunguka akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali wa Europa League dhidi ya Atletico Madrid, utakaochezwa kesho kaskazini mwa jijini London.
Wenger amesema mpango wa kutangaza kupitia mkutano na waandishi wa habari wa mwishoni mwa juma lililopita, haukutoka moyoni mwake moja kwa moja.
Babu huyo mwenye umri wa miaka 68, amesema kuna mambo mengi nyuma ya pazia ambayo yalimsukuma kutoa kauli ya kung’atuka itakapofika mwishoni mwa msimu huu, lakini lengo lake kubwa lilikua ni kuendelea kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Arsenal hadi mkataba wake ungefikia kikomo mwaka 2019.
“Nimekua na malengo makubwa na klabu hii, na lengo langu ni kuitumikia siku hadi siku, lakini imenibidi kutangaza kukaa pembeni kutokana na mipango iliyowekwa na viongozi wa ngazi za juu.” Amesema Wenger.
“Nilipanga kufanya kazi hapa kwa mujibu wa mkataba wangu unavyonielekeza, nilistahili kuondoka mwaka 2020, lakini pamoja na yote hayo nimeafiki kuondoka mwishoni mwa msimu huu, kwa maslahi ya klabu na sio yangu binafsi.” Aliongeza mzee huyo
Chini ya utawala wake ulioanza mwaka 1996, Arsenal imebahatika kutwaa ubingwa wa ligi ya England mara tatu na kombe la chama cha soka nchini humo (FA Cup) mara saba. Katika mafanikio hayo, Wenger alitwaa mataji hayo kwa pamoja mwaka 1998 na 2002.
Tayari idadi kubwa ya mameneja imeanza kutajwa katika vyombo mbalimbali vya habari katika mchakato wa kumsaka mrithi wa Arsene Wenger, na miongoni mwa wanaotajwa yupo aliyekua meneja wa FC Barcelona Luis Enrique pamoja na nahodha wa zamani wa Arsenal Patrick Vieira.
Hata hivyo Wenger alipoulizwa ni nani angependa kuona akimrithi klabuni hapo, alijibu hapendi kuingia katika mkumbo huo, japo anavutiwa na Luis Enrique, kutokana na mafanikio alioyapata kwa muda mfupi akiwa FC Barcelona.
Mtendaji mkuu wa Arsenal Ivan Gazidis, mwanzoni mwa juma hili alizungumza katika mkutano na waandishi wa habari na kuahidi suala la kutangazwa kwa meneja mpya litafanywa haraka iwezekanavyo.