Mazungumzo yameanza mjini Antananarivo kati ya chama tawala na upinzani Kufuatia maandamano yaliyokuwa yanafanywa na wafuasi wa upinzani wakiandamana tangu siku ya Jumamosi wiki iliyopita kuelekea makao makuu ya Mahakama ya Katiba mjini Antananarivo na kumtaka Rais Hery Rajaonarimampianina kujiuzulu miezi michache kabla ya Uchaguzi mkuu.
Taarifa hiyo imethibitishwa na Kiongozi wa Chama Tawala cha HVM, Rivo Rakotovao, ambaye amesema mkutano wa mazungumzo umefanyika kati ya chama tawala na wapinzani jana (Jumatano) jioni katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Antananarivo.
”Majadiliano kati ya wabunge wa upinzani na Bw Rakotovao ambapo Jumuiya ya kimataifa kupitia Umoja wa Afrika umealika wadau katika mgogoro huo kuketi kwenye meza ya mazungumzo,” amesema Augustin Andriamananoro, mshirika wa karibu wa Andry Rajoelina, mmoja wa viongozi wa upinzani.
“Umoja wa Afrika unatafuta njia ya upatanisho ili kuondokana na mgogoro huo mara moja,” ameongeza.
Mgogoro huu mpya nchini Madagascar, kisiwa kikubwa katika Bahari ya Hindi chenye historia ya kisiasa yenye utata, ulianza siku ya Jumamosi kwa maandamano ya upinzani ambayo yalisababisha makabiliano na polisi. Watu wawili waliuawa.
Upinzani ulitoa wito wa kuandamana kupinga sheria mpya za uchaguzi ambazo zinaonekana kuegemea upande wa serikali.
Tangu wakati huo, maandamano yanaendelea kila siku katika mji mkuu wa nchi hiyo, kwa kauli mbiu mpya: kupata hakikisho la kujiuzulu kwa rais, madarakani tangu mwaka 2014.