Kiungo kutoka nchini Rwanda Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema endapo kikosi cha Simba kitaibuka na ushindi dhidi ya Young Africans siku ya jumapili Uwanja wa Taifa Dar es salaam, watakuwa wamekaribia kabisa kutwaa ubingwa msimu huu.
Niyonzima amesema hayo, huku akifahamu fika hatokua sehemu ya kikosi cha Simba ambacho kitashuka dimbani kukabiliana na mahasimu wao siku hiyo, kufuatia kupata msiba wa dada yake.
Kiungo huyo ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Young Africans, tayari ameshaondoka nchini na kurejea nyumbani kwao Rwanda.
Licha ya kutokuwa sehemu ya mchezo huo, Niyonzima amesema wachezaji wengine watakaopata nafasi kushuka dimbani, anaamini watapeperusha vizuri bendera ya Simba na ushindi utapatikana.
“Ni mchezo muhimu kwetu, kama tutapata ushindi tutakuwa kwenye mazingira mazuri ya kuchukua ubingwa msimu huu.
“Mimi sitakuwepo katika mchezo huo nimepata msiba wa dada yangu lakini naamini yoyote atakaye pewa nafasi atafanya vizuri na tutashinda mchezo,” alisema Niyonzima.
Endapo Simba itaibuka na ushindi katika mchezo huo itaendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya alama 14, na kuongeza mshawasha kwa mahasimu wao ambao wanahaha kusaka namna ya kutetea taji lao msimu huu.