Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, watamkosa mshambuliaji wao wa pembeni Arjen Robben katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid, utakaochezwa kesho mjini Madrid, Hispania.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Uholanzi ameshindwa kufikia viwango vya kitabibu, baada ya kufanyiwa vipimo vya mwisho na jopo la madaktari kuelekea katika mchezo huo, ambao utaamua nani atakwenda fainali msimu huu.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alishindwa kuendelea na mchezo wa mkondo wa kwanza baada ya kuumia mguu dakika ya nane kipindi cha kwanza, na alitarajiwa huenda angekuwa na nafasi ya kucheza dhidi ya Real Madrid hapo kesho.
Hata hivyo wachezaji David Alaba aliekua anasumbuliwa na maumivu ya Paja pamoja na kiungo Javi Martinez aliekua na maumivu ya kichwa, wanapewa nafasi kubwa ya kucheza katika mchezo huo.
Kwa upande wa Real Madrid beki wa kuliwa Dani Carvajal yupo kwenye mashaka ya kuukosa mchezo wa kesho, kufuatia jeraha la nyama za paja alilolipata katika mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Munich, huku kiungo mshambuliaji Isco akitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi, licha ya kuripotiwa kuumia bega mazoezini.
Real Madrid watakua kwenye uwanja wa nyumbani, huku wakichagizwa na ushindi wa mabao mawili kwa moja waliouvuna mjini Munich juma lililopita, huku FC Bayern Munich watakua na kazi ya kuhakikisha wanasaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuendelea, endapo watahitaji kucheza hatua ya fainali.