Serikali imetambulisha chanjo ya bure ya dawa ya kinga ili kuzuia mtu asipate maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), utambulisho huo umefanyika jijini Mbeya ukiwa umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa mashirika binafsi yanayojihusha na masuala ya Ukimwi.
Mkurugenzi wa asasi iitwayo HJFMRI ambayo ndiyo iliyopewa kazi ya kusambaza dawa hizo kwa niaba ya serikali, Joseph Chintowa, amesema dawa hiyo ina uwezo wa kumkinga mtu asipate maambukizi ya VVU kwa zaidi ya asilimia 90, ikiwa itatumika kwa ufasaha.
Amesisitiza kuwa mtu anayestahili kutumia dawa hiyo ni yule aliyepima na kuonekana hana maambukizi ya VVU, lakini yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi.
“Kabla ya kutumia dawa hizi unatakiwa kupimwa na ikionekana hujaambukizwa, unakuwa na sifa ya kutumia dawa kinga, na wale ambao watabainika kuwa tayari wana maambukizi, hawastahili kutumia dawa hizi badala yake watapewa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) kwa ajili ya kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi.”amesema Chintowa na kuongeza.
Aidha, ameongezea kuwa kwa kuanzia chanjo hii ya dawa kinga itaanza kutolewa kwa watu walio kwenye makundi hatarishi ya kupata maambukizi mapya kama vile watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, mabinti wanaofanya biashara ya ngono na watu wanafanya mapenzi ya jinsia moja.
Hata hivyo Serikali imesema chanjo hiyo dhidi ya Virusi vya Ukimwi itaanza kutolewa katika mikoa ya Mbeya na Songwe.