Rais wa Marekani, Donald Trump amekutana kwa mara ya kwanza na raia watatu wa nchi hiyo walioachiwa huru baada ya kufungwa kwa miaka mitatu nchini Korea Kaskazini.
Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa wafungwa hao wameachiwa huru ikiwa ni ishara ya nia njema ya mkutano kati ya rais Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ili kumaliza mgogoro uliokuwepo kati ya mataifa hayo kuhusu mpango wa silaha za kinyuklia.
Watu hao waliwasili Washington kwa ndege maalum, mwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Ikulu hiyo.
Trump amesema kuwa hatua hiyo ni ishara kuwa mkutano wake na Kim Jong-un utafanikiwa kwa kiwango kikubwa na utazinufaisha nchi hizo pamoja na Korea Kusini.
“Hakika hatukudhani kama hili[la kuwaachia hawa raia wa Marekani] lingefanyika mapema hivi kabla ya mkutano wetu,” Trump anakaririwa.
Alipoulizwa kama hatua hiyo anaichukulia kama moja kati ya mafanikio yake makubwa kwenye mgogoro wa Penisula ya Korea, alisema “hii ni heshima kubwa. Lakini heshima ya kweli itakuja kama tutafanikiwa kuondoa kabisa mpango wa silaha za nyuklia katika eneo lote la Korea.”
Alisisitiza kuwa mkutano wake na kiongozi wa Korea Kaskazini anaamini utafanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuweka historia ya aina yake.