Jeshi la Magereza Tanzania limetoa taarifa rasmi juu ya kuachiwa huru kwa msanii wa maigizo nchini Elizabeth Michael maarufu kama Lulu ikidai kuwa Mahakama imebadilisha adhabu na kufanya atumikie kifungo cha nje kwa kufanya huduma kwa jamii yaani Community Service.
Pia taarifa hizo zimeeleza sababu za kuachiwa kwa Lulu kuwa ni kutokana na msamaha wa Rais John Magufuli uliotolewa siku ya Maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ambapo wafungwa wote wenye vigezo walipata msamaha wa 1/4 ya adhabu yao.
”Lulu kwa sababu ni moja yawafungwa walionufaika na msamaha wa Rais, baada ya msamaha wa rais alitakiwa atoke mwezi wa 11 mwaka huu tarehe 12 lakini kwa amri ya mahakama kwa kutumia kifungu nilichokitaja cha ”Community Service” ametoka Mei 12, 2018 ataendelea kuhesabika kama mfungwa mpaka hiyo tarehe 12 mwezi 11 lakini badala ya kuwa gerezani atatumikia kifungo chake adhabu kwa kufanya huduma ya jamii” amesema Augustino Mboje.
Mbali na Lulu Michael Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia tiketi ya Chagema, Joseph Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga pia walinufaika na msamaha huo mara baada ya kutiwa ndani kwa kashfa ya kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais John Pombe Magufuli.