Hatimaye kesho Dunia itashuhudia ndoa na sherehe ya harusi ya kihistoria ya Kifalme, kati ya Prince Harry wa Uingereza na aliyekuwa muigizaji kutoka Marekani, Meghan Markle huku bajeti iliyotengwa ikizua gumzo la mwaka.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza na Marekani ikiwa ni pamoja na mtandao maarufu unaoangazia gharama za masuala ya ndoa na sherehe za harusi wa bridebook, bajeti ya tukio hilo la kifahari ni $45 milioni, ambazo ni zaidi ya sh.102.6 bilioni za Tanzania.
Imeelezwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha zilizotengwa kitatumika kuimarisha ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuwalipa wadunguaji, mashushu na wanausalama wengine watakaohakikisha familia hiyo ya kifalme pamoja na wageni waalikwa wako salama.
Gharama nyingine za kawaida lakini zilizochukua kiasi kikubwa cha fedha ni vinywaji, vyakula, mapambo, usafiri, mazingira ya choo za kifahari n.k.
Ingawa kwa kufuata utaratibu wa kitamaduni wa kifalme, gharama za ndoa zilipaswa kulipwa na upande wa bibi harusi, katika ndoa hii, gharama zitalipwa na familia hiyo ya kifalme huku nyingine zikiwa sehemu ya fedha za walipa kodi.
Hata hivyo, taarifa za ndani zimeeleza kuwa bibi harusi mtarajiwa atagharamia shela atakayoivaa kesho, kama gharama pekee, gharama nyingine Himaya ya Mfalme ya Kensington itakamilisha.
Prince Harry na Meghan Markle wanatarajiwa kufunga ndoa yao kesho katika kanisa la Mtakatifu George lililoko Windsor. Baadaye, sherehe za harusi zitahamishiwa katika eneo la kifalme la Windsor Castle.
Ingawa kuna mfanano wa matukio katika ndoa hii na ile ya Kate Middleton na Prince Williams ya mwaka 2011, ndoa hii itakuwa na gharama kubwa zaidi. Kate Middleton na Prince Williams walitumia $34 milioni. Lakini kitu cha kufanana ni kwamba Kate Middleton pia alijinunulia shela yake kama gharama pekee alizohusika nazo.