Kuendelea kufanya vibaya kwa kikosi cha mabingwa wa zamani wa Tanzania bara Young Africans, kumewafanya wadau soka nchini kuwa katika hali ya taharuki, huku wakijiuliza kulikoni ndani ya kikosi cha wababe hao ambao walitamba, na kujiita WA KIMATAIFA.
Kikosi cha Young Africans kimedhihirisha bado hakipo vizuri, baada ya jana jumapili (Juni 03-2017) kufungwa mabao matatu kwa moja, katika mchezo wa kuwania ubingwa wa Sport Pesa Super, dhidi ya Kakamega Home Boys Cup na kujikuta wakitupwa nje mapema.
Afisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara Masau Bwire, ni mmoja wa wadau wa soka nchini walioonyesha hisia zao baada ya kikosi cha Young Africans kuendelea kufanya vibaya na kujikuta akiandika makala fupi, ambayo ndani yake ina ushauri mzuri kwa wachezaji, viongozi, mashabiki na wanachama.
Bwire anaamini ushauri wake ukifuatwa na wahusika hao wa Young Africans, watafanikiwa kupita katika kipindi hiki kigumu, na nyakati za furaha kama ilivyokua zamani zitarudi klabuni kwao.
Masau Bwire ameandika: Young Africans mshikamane, msikimbiane wakati wa shida.
Shida haina adabu, inadhalilisha, inaudhi, inakosesha furaha, amani, inakuondolea thamani na utu kwa watu, shida ni kitu kibaya mno, usiombe ikutokee, wala usimcheke mwenye shida maana ipo siku, itahamia kwako, utajuta kuzaliwa, haina adabu hii, leo kwake, kesho kwako, hivyo, tusichekane wakati wa shida, tuhurumiane na kufarijiana sisi kwa sisi.
Wakati wa shida utamjua ndugu, rafiki wa kweli, utamjua mnafiki, ambaye shida ikikutokea anakataa undugu, siyo rafiki yako tena, kutwa kukusimanga tu kwa watu, shida wakati fulani ni makusudi ya Mungu kutaka ujue utu wa watu kwako, lakini pia shida ni kipimo kinachokuonesha ndugu na rafiki wa kweli, wanafiki utawajua wakati wa shida!
Hakuna wakati unaohitaji uvumilivu, ‘kuziba masikio’, ushirikiano na mshikamano kama wakati wa shida, ni hivi tu vitakuondolea shida inayokutesa kwa wakati wako, shida haikimbiwi, inakabiliwa, tena ikikabiliwa kwa pamoja, itatoweka haraka, hali ya kawaida itarudi, tena kwa ufanisi mkubwa pengine kuliko mafanikio kabla ya shida hii!
Ndugu zangu, rafiki zangu wana wa Jangwani, Young Africans, poleni sana, mpo kwenye kipindi kigumu sana, kipindi cha shida kubwa, kipindi ambacho mnatakiwa msimame imara sana kukabiliana na shida hii ili iondoke, ni cha mpito tu, Mungu ni wa wote, mkipambana, atawaonesha njia ya kutokea, mambo yatakuwa mwemwelemwemwele, mtafanikiwa sana!
Ushauri wangu kwenu, shikamaneni, msinyosheane vidole, msilaumiane wala kutafutana uchawi, kuweni kitu kimoja, mjadili, mshauriane kwa pamoja, kamwe msikimbiane, simameni imara muikabili hali hii kwa pamoja.
Nimesema awali, shida ni kipimo cha utu wa mtu, kukuonesha ndugu, rafiki wa kweli na wanafiki, wanaokukimbieni wakati huu wa shida, hao Mungu anakuonesheni kwamba, siyo wote waliomo katika zizi ni wa zizi hili, waacheni waende maana mlikuwa nao zizini kumbe hawakuwa wa zizi hili!
Kwa niaba ya Ruvu Shooting, tunawaombea kwa Mungu, kwa moyo wa upendo na wa dhati kabisa shida hii inayotokana na ukata, iwaondoke kabla ya msimu mpya wa ligi 2018/19, mpate mahela mengi, muwe katika hali yenu ya miaka ya nyuma, umataifa wenu uonekane, tena kwa kasi, sisi hatuwaombei njaa, tunawaombea mafanikio ili tuwapapase maana, msimu uliomalizika 2017/18 tuliwahurumia kuwapapasa kutokana na shida mlionayo tukitekeleza agizo la Mungu, “Hurumianeni, farijianeni ninyi kwa ninyi”.
Young Africans daima mbele, nyuma mwiko…..
Masau Bwire – Mzalendo.