Kiungo kutoka nchini Brazil Frederico Rodrigues de Paula Santos (Fred), leo jumatatu atafanyiwa vipimo vya afya na jopo la madaktari wa klabu ya Man Utd, ili kukamilisha uhamisho wake kutoka Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Televisheni ya Sky Sports imeripoti kuwa, kiungo huyo ambaye aliitumikia timu yake ya taifa katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Croatia, huenda akawa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Jose Mourinho katika kipindi hiki.
Kituo hicho cha televisheni kimebaini kuwa, mazungumzo ya usajili wa Fred, yalianza tangu mwezi Mei, baada ya wang’amuzi wa vipaji wa Man Utd kumfuatilia na kuridhishwa na kiwango chake.
Hata hivyo mwezi Januari, Fred almanusura ajiunga na wapizani wa Mashetani Wekundu Man City, lakini mipango ya uhamisho wake ilikwama.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, alisajiliwa na Shakhtar mwaka 2013 akitoke nchini kwao Brazil alipokua akiitumikia klabu ya Internacional, na tayari ameshacheza michezo 150 akiwa na klabu hiyo ya nchini Ukraine.
Mara baada ya mchezo dhidi ya Croatia, kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil Tite aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hajashangazwa na mpango wa Man Utd kumsajili Fred, kwani alitambua uwezo na kipaji cha mchezaji huyo vitamuondoa katika ligi ya Ukraine na kumpeleka kwenye ligi kubwa duniani.
“Wakati jambo hili linatokea, sikushtushwa kabisa, kwa sababu nilijua ipo siku Fred ataondoka Ukraine na kwenda katika ligi kubwa duniani kama ligi ya England,”
“Fred ana uwezo mkubwa kisoka na ninatarajia makubwa zaidi kutoka kwake, endapo atakamilisha ndoto za kujiunga na Man Utd.” Alisema Tite.
Kikosi cha Brazil kitacheza mchezo mwingine wa kirafiki Juni 10 dhidi ya Austria mjini Vienna, kabla ya kuanza safari ya Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia. Brazil imepangwa kundi E na timu za mataifa ya Uswiz, Costa Rica na Serbia.