Msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz amemshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuendelea kuwa hai mara baada ya kupoteza fahamu kwa muda wa siku saba akiwa nchini Afrika Kusini baada ya kufanyiwa upasuaji.
Dimpoz ametumia mtandao wa Instagram kuwajuza mashabiki wake kuhusu tatizo la kiafya lilihusisha koo lake kushindwa kupitisha chakula. Amesema kuifikia leo ilitokana na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu kwani ingeweza kuwa ‘vinginevyo’.
“Namshukuru Mungu kwa kuweza hata kufika siku ya leo manake hali ilikuwa mbaya sana, lakini kikubwa zaidi ni uzima na ninamshukuru Mungu zaidi kuwa uzima bado upo, tatizo lilikuwa hivi napata tabu sana nilikuwa nikila chakula hakishuki hata kwenye maji pia [nilikuwa siwezi kunywa],” amesema Ommy Dimpoz.
“Nilikuwa naumwa nimefanyiwa oparesheni kubwa, kwahiyo nimetumia kama siku 15 hospitali, lakini namshukuru Mungu nimetoka sasa hivi na ‘i hope i will come back stronger now'(natumaini nitakuwa imara zaidi ), nipo kwenye mapumziko ya kurejesha afya yangu,” aliongeza.
Mashabiki wa muziki pamoja na wasanii mbalimbali wamempa pole msanii huyo ambaye wimbo wake wa ‘Yanje’ aliouachia wiki kadhaa zilizopita unaendelea kufanya vizuri na kushika nafasi za juu kwenye chati mbalimbali za muziki nchini.