Mshambuliaji wa Manchester United Anthony Martial, anakaribia kujiunga na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus, baada ya kuwekwa sokoni.
Martial yu njiani kuondoka Old Trafford, baada ya kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho, tofauti na ilivyokua katika utawala wa meneja Louis Van Gaal ambaye alimsajili akitokea AS Monaco ya Ufaransa.
Kusajiliwa kwa mshambuliaji Alexis Sanchez klabuni hapo mwezi januari, pia kuliongeza changamoto kwa Martial kuendelea kusota kwenye benchi la wachezaji wa akiba.
Taarifa kutoka nchini Italia zinaeleza kuwa, Martial ameshafanya mazungumzo na viongozi wa Juventus na kuafiki makubaliano binafsi ya kimslahi, na jambo linalosubiriwa kwa sasa ni kupimwa afya yake na kutambulishwa mbele ya waandishi wa habari.
Hata hivyo mpaka sasa ada ya uhamisho wa mshambuliaji huyo aliyeachwa kwenye kikosi cha Ufaransa kinachoshiriki fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi haijatajwa, huku baadhi ya vyombo vya habari vya italia vikiripoti huenda akawasajiliwa kwa Pauni milioni 80.