Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayowakabili Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti chama hicho, Freeman Mbowe hadi June 27,2018 kwa sababu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Vicent Mashinji hakufika mahakamani.
Hayo yamejiri leo Juni 25, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi kueleza kuwa kesi hiyo imeitishwa ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali lakini mshtakiwa wa 6 ambaye ni Dkt. Vicent Mashinji hayupo mahakamani, ambapo Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa Dkt. Mashinji ana udhuru yupo katika mahakama ya Songea ana kesi nyingine, hivyo wanaomba ahirisho.
Mara baada ya wakili Kibatala kutoa maombi hayo ya kutaka kuahirishwa kwa kesi hiyo, uliibuka mvutano wa kisheria baada ya wakili wa Serikali, Paul Kadushi kutaka kesi iahirishwe hadi kesho, huku wakili Kibatala akitaka iahirishwe hadi tarehe nyingine, ambapo hatimaye Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi June 27, 2018
Washtakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba, John Mnyika.
Pamoja na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, ambapo inadaiwa February 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi tamko lililowataka kutawanyika February 16, 2018 katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.
Washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo Mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Afisa wa polisi SSP, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani ambao ulipeĺekea hofu na hatimaye kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.