Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amekabidhi hati ya nyumba kwa familia ya Zainabu Kaswaka iliyoteseka na kusababisha ugonjwa wa kupooza kwa mume wake baada ya nyumba na ardhi yao kuuzwa baada ya matapeli kutumia hati ya nyumba yao kuchukuwa mkopo Bank ya FNB pasipo familia kujua.
Upatikanaji wa hati hiyo umekuja baada ya majadiliano ya kina baina ya Makonda, Wanasheria na Bank ya FNB iliyotoa mkopo ambapo baada ya mkuu wa mkoa kuagiza kufanyika uchunguzi Bank ilibaini uzembe wa baadhi ya watumishi wa Bank hiyo uliopelekea kasoro hiyo.
Makonda pia amefanikiwa kumhakikishia makazi ya kudumu Mama Mjane, Benadetha Rwendera alietakiwa kuondoka kwenye nyumba yake na kujikuta akilala nje baada ya kununua eneo na kujenga nyumba pasipokujua kuwa aliemuuzia eneo tayari alikuwa amechukuwa Mkopo Bank ya KCB jambo lililopelekea nyumba kuvunjwa na kuuzwa.
Baada ya majadiliano baina ya Makonda na Bank ya KCB waliafiki kwa pamoja kumuachia mjane aendelee kuishi wakati kesi ikiendelea mahakamani na pindi hukumu itakapotoka utafanyika mgawanyo wa ardhi.
Aidha, Makonda amesema hadi sasa Mkoa umefanikiwa kusikiliza kesi za wananchi zaidi ya 1,028,000 ambapo kesi zilizotatuliwa ofisini kwake ni 628,000 na kesi zilizokwenda mahakamani ni 60 ambapo Kati ya hizo kesi 17 zimeshatolewa hukumu na watu kupata haki zao chini ya usimamizi wa ofisi ya Makonda kupitia msaada wa mawakili waliowasimamia bila malipo.
Itakumbukwa Makonda aliahidi kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kulipa mawakili bure na haya ndio matunda yake.