Raia wa Tunisia ambaye alifanya kazi kama mlinzi binafsi wa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda, Osama bin Laden ambaye alishikiliwa nchini Ujerumani Jumatatu wiki hii amepata pigo baada ya kutakiwa kuondolewa nchini humo.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama wa Ujerumani, mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Sami. A aliishi nchini humo kwa zaidi ya miaka 20 lakini uwepo wake uliibua taharuki zaidi hivi karibuni, ingawa alikuwa chini ya uangalizi maalum wa jeshi la polisi.
Awali, Sami A mwenye umri wa miaka 41, alifanikiwa kuishawishi mahakama dhidi ya uamuzi wa kumfukuza nchini humo na kumrejesha nchini Tunisia akidai kuwa angekuwa kwenye hatari ya kukamatwa na kuteswa akiwa nchini kwake.
Lakini, Idara ya Uhamiaji ilibadili uamuzi huo kutokana na malalamiko mengi ya wananchi pamoja na kauli ya waziri wa mambo ya ndani, Horst Seehofer.
“Hatimaye ataondolewa nchini,” kinasomeka kichwa cha habari kuu ya gazeti la Bild ambalo lilitoa habari hiyo kwa mara ya kwanza.
Msemaji wa Serikali eneo la Magharibi mwa Ujerumani amekaririwa na shirika la habari la AFP akieleza kuwa Sami A anashikiliwa na jeshi hilo akisubiri kusafirishwa kwenda Tunisia.
Raia huyo wa Tunisia aliwasili Ujerumani mwaka 1997, alipewa masharti ya kuripoti polisi kila siku katika kipindi chote akiwa nchini humo, ili kufuatilia mienendo yake kwa karibu, lakini hakuwahi kufunguliwa mashtaka. Amekuwa akikanusha kuwa mlinzi wa Osama.
Mwaka 2015, Jaji wa Mahakama Kuu ilisema kuwa inaamini Sami A alishiriki mafunzo ya kijeshi kwenye kambi ya A-Qaeda nchini Afghanistan mwaka 1999 na 2000 na kwamba alikuwa miongoni mwa walinzi binafsi wa Osama.