Nyota wa mpira wa kikapu wa NBA, LeBron James amejiunga rasmi na Los Angeles Lakers na kuachana na timu iliyomlea ya Cleveland Cavaliers maarufu kama The Cavs.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 anayetajwa kuwa mchezaji bora zaidi wa kikapu duniani, amewekewa mezani kiasi cha $154m kilichyomvuta kusaini mkataba mpya.
James ambaye alikuwa huru tangu Julai Mosi mwaka huu, ameweka wazi uamuzi wake huo kupitia mtandao wa Instagram.
“Asante ‘Northeast Ohio’ kwa misimu minne mizuri. Hapo patakuwa nyumbani siku zote,” aliandika James ambaye sasa anahamia Los Angeles, California.
Bingwa huyo mara tatu wa ligi ya NBA alichaguliwa na The Cavs mwaka 2003 na kufanikiwa kuibuka kuwa mchezaji bora zaidi. Alitajwa kuwa mchezaji wa NBA mwenye thamani zaidi mwaka 2009 na mwaka 2010. Lakini mwaka 2010, alihamia Miami katika uamuzi ambao ulizua utata.
Alifanikiwa kuchukua ubingwa mwaka 2012 na kushika nafasi ya pili mwaka uliofuata. Baada ya mafanikio hayo, aliamua kurejea tena Cleveland.
Mchango wake uliisaidia Cleveland kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016 ikiivuruga Golden State. Ubingwa huo kwa Cleveland ulikuwa wa kwanza ndani ya kipindi cha miaka 52.
Lebron James ametajwa kuwa ndiye mchezaji wa pili kwa umaarufu zaidi duniani kwa mwaka 2018 kwa mujibu wa ESPN, akimfuatia Cristiano Ronaldo.