Kamati kuu ya shirikisho la soka nchini Hispania iliyokutana leo saa tano na nusu kwa saa za nchi hiyo, imefikia maamuzi ya kumteua Jose Francisco Molina, kuwa mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho hilo.
Molina mwenye umri wa miaka 47, ameteuliwa kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Fernando Hierro ambaye alitangaza kujiuzulu, baada ya kurejea na kikosi cha Hispania, ambacho alikiongoza kama kocha wa muda kwenye fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi.
Molina ambaye aliwahi kuwa meneja wa klabu za Villarreal na Atletico Kolkata anatarajiwa kutangazwa mbele ya waandishi wa habari wakati wowote kuanzia sasa.
Mbali na kukumbukwa katika nafasi ya ukufunzi wa soka, mkurugenzi huyo mpya wa ufundi, aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Hispania katika nafasi ya mlinda mlango wakati wa fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 1996 (Euro 96), pamoja na fainali za kombe la dunia mwaka 1998 na 2000.
Msimu wa 1995/96, akicheza kwenye klabu ya Atletico Madrid, alitwaa tuzo ya Zamora kufuatia kuwa mlinda mlango aliyeruhusu mabao machache.