Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ofisi za maafisa ugani zinapaswa kuwepo walipo wakulima, wafugaji na wavuvi na kwamba maafisa ugani katika ngazi zote lazima wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu.
Majaliwa amesema hayo Julai 12, 2018 wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa maafisa kilimo, mifugo na uvuvi kutoka Tanzania Bara ulioanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma. Mkutano huo unahudhuriwa na washiriki 570.
“Maafisa ugani katika ngazi zote lazima wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu kutekeleza majukumu yao. Wataalam wa Wizara washuke hadi ngazi ya mikoa na Halmashauri kusaidiana na waliopo kwenye ngazi hizo.
Amesema wakulima, wafugaji, na wavuvi hawana budi kupatiwa mbinu bora kuanzia hatua ya uzalishaji hadi kupata masoko ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi zenye tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Pia, amesisitiza kwamba maafisa ugani ni lazima wawe na orodha sahihi ya wakulima, wafugaji na wavuvi wote kuanzia ngazi ya kitongoji na aina ya mazao wanayoshughulikia, malengo ya uzalishaji na utekelezaji.
“Maafisa ugani wawe na takwimu sahihi za aina na kiasi cha mahitaji ya teknolojia na pembejeo za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yao lakini pia wasaidie kuunganisha vikundi vya wakulima, wafugaji, wavuvi na kuunda ushirika imara ili kuendeleza juhudi za kufufua ushirika kama mkombozi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.”
Aidha, Waziri Mkuu amewataka maafisa ugani waende wakasimamie mifumo rasmi ya ununuzi wa mazao ili kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri za mazao yao.
“Hatutaki kusikia watu wanatumia mifumo isiyo rasmi kama chomachoma(kwenye ufuta), butura (kahawa huko Karagwe), katakichwa (kahawa Moshi), kangomba (korosho) na vishada (tumbaku). Nenda kapambane nao, wewe ni afisa wa Serikali na hupaswi kuacha wananchi wanateseka,” alisema.
“Nenda kahimize mfumo wa kuuza mazo kwa ushirika badala kuruhusu wanunuzi kwenda kwa mkulima mmojammoja. Pia mtusaidie kufafanua dhana ya Stakabadhi za mazao Ghalani kwamba siyo malipo ya papo kwa papo. Muwaeleze wakulima kwamba wanapeleka mazao pake wakati wakisubiria bei iwe nzuri, siyo kwamba wanakopwa,” amesisitiza.