Katibu Mwenezi wa chama wa Chama cha Mapinduzi CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho hakina wasiwasi wa aina yoyote na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika uchaguzi mdogo wa marudio ya Ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma huku akieleza kuwa wanaoitilia shaka tume hiyo ndiyo wenye matatizo.
“Sisi hatuna mashaka yoyote na Tume ya Uchaguzi (NEC) na kama tungekuwa nayo basi tungeshayaeleza mahali husika ila ukiona mtu anajitokeza barabarani na kusema kuna changamoto bila ya kuzipeleka sehemu husika basi ujue yeye ndiyo mwenye changamoto na siyo Tume”, amesema Polepole.
Polepole ameendelea kusema CCM imejiwekea rekodi ya kushughulika na shida za watu na kutatua kero za wananchi wa Tanzania na hili limefanyika vizuri sana chini ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. John Magufuli.
“Tumekuwa hatuna mzaha, masihara na watu wanaocheza na rasilimali za umma, wanaonyanyasa wananchi, wasiowajibika na kushughulika na shida za watu na kwa rekodi ambayo tumeshajiwekea mpaka sasa hivi tutaenda kupata ushindi mkubwa wa kishindo kwasababu ya kazi ile nzuri ambayo tumekwisha ifanya hadi sasa hivi”.
Aidha, siku tatu zilizopita, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa kauli yake iliyokuwa ikiitaka NEC kuendesha uchaguzi huo kwa uhuru na haki kuwa kuna baadhi ya vitu wamevibaini vikiendeshwa ndivyo sivyo.
Uchaguzi huo mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Agosti 12 mwaka huuu baada ya kuwepo wazi Jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma kufuatia Mbunge Kasuku Bilago kufariki dunia mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu pamoja na madiwani wa maeneo mbalimbali kuyaacha majimbo yao na kujiunga CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli.