Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo rasmi ya kiserikali na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye yuko hapa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Viongozi hao wawili, kwa pamoja, leo mchana Julai 22, 2018 wameshuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi (diplomatic and service passports).
Uwekaji saini huo ulifanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga na Makamu wa Kwanza Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bw. Lim Sung-nam kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari waliohudhuria hafla ya uwekaji saini, Waziri Mkuu amesema kwenye mazungumzo yao wamejadiliana mambo mengi ambayo yamelenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
“Tumejadili namna ya kuimarisha mahusiano yetu kidiplomasia; kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchumi na maendeleo; ushirikiano katika elimu, sayansi na TEHAMA ushirikiano katika sekta ya utamaduni na utalii,” amesema.
“Pia tumeongelea fursa ya mradi mkubwa wa reli, ujenzi wa daraja la Salender, mradi wa hospitali ya Mloganzila; mradi wa NIDA ambao tumepata mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kuendelea kutoa vitambulisho vya uraia; ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa mita 3,200; ujenzi wa barabara ya Kazirambwa – Chaya yenye urefu wa km. 42 na uimarishaji wa sekta ya afya kwa kujenga hospitali tano za rufaa kwenye kanda zetu,” amesema.
Waziri Mkuu amesema amewaalika makampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea yaje kuwekeza nchini ili kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. “Pia wafanyabiashara aliokuja nao, kesho watashiriki kongamano la kibiashara baina ya Korea na Tanzania ili waweze kubadilishana uzoefu na wenzao wa Tanzania.”
“Tumewaomba pia watangaze vivutio vya utalii vya hapa nchini huko kwao na Balozi wetu wa Tanzania huko Korea atasimamia utangazaji wa vivutio vya hapa nchini kwetu. Sisi pia tumewapongeza kwa uamuzi wa Korea Kusini kukaa pamoja na Korea Kaskazini na kuimarisha amani kwa nchi zao,” amesema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele; Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani; Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ally; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Bw. Issa Gavu na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya. Wengine ni Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali na wakuu wa taasisi.
Waziri Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Jamhuri ya Korea ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na mikopo ya masharti nafuu ikiwemo misaada ya fedha katika bajeti, ujenzi wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, wataalamu wa kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Baadhi ya miradi ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi wa kuboresha Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi wa Mfumo wa Usajili wa Meli na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar, Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto Malagarasi.
Vile vile, Korea ni mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la Afrika ambapo hivi karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika (KOAFEC VI) uliofanyika Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali ya Korea ilitangaza msaada wa dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la Afrika kwa kipindi cha 2018-2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na msaada huo.