Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wamemsajili mshambuliaji kinda kutoka nchini Canada Alphonso Davies akitokea klabu ya Vancouver Whitecaps inayoshiriki ligi kuu ya Marekani (MLS).
Usajili wa kinda huyo mwenye umri wa miaka 17, umevunja rekodi kwa klabu zinazoshiriki ligi ya Marekani ukanda wa kaskazini.
Uongozi wa Whitecaps umethibitisha kuuzwa kwa mchezaji huyo, ambaye ada yake ya usajili imetajwa kuwa dola za kimarekani milioni 22.
Davies, ambaye ni mzaliwa wa Ghana, tayari ameshaifungia Whitecaps mabao 20 katika msimu wa ligi ya MLS unaoendelea.
“Alphonso Davies ni mchezaji mwenye kiwango cha hali ya juu,” alisema mkurugenzi wa michezo wa FC Bayern Munich Hasan Salihamidzic alipohojiwa na mwandishi wa habari za Tovuti ya klabu hiyo.
“Kwa umri wake wa miaka 17, ni ajabu kuona mchezaji anacheza soka kwa kiwango cha hali ya juu, tumekamilisha usajili wake, tunaamini atakapokua nasi ataonyesha uwezo mkubwa kisoka na kufanikisha malengo tuliyojiwekea kwa miaka ijayo. ”
Davies, atakaefikisha umri wa miaka 18 mwezi Novemba, amejiunga na FC Bayern Munich kwa kusaini mkataba ambao utadumu hadi mwezi Juni mwaka 2023.
Atajiunga rasmi na mabingwa hao wa Ujerumani mwezi Januari mwaka 2019, baada ya kukamilika kwa msimu wa ligi ya Marekani MLS.