Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change (MDC) kimedai kuwa mgombea wake, Nelson Chamisa ameshinda uchaguzi wa urais uliofanyika jana.
MDC wamedai kuwa wamefanya hesabu za kura zote kwenye vituo husika na wamebaini kuwa wameshinda na kwamba chama tawala cha Zanu-PF kinajaribu kufanya mbinu za kuchakachua matokeo kwa kuyachelewesha.
“Tumekusanya matokeo kutoka kwa mawakala wetu wote kwenye vituo vya kupigia kura na kinachoonekana ni dhahiri kuwa mgombea urais kwa tiketi ya MDC, Nelson Chamisa ameshinda. Tunaitaka Tume kuweka wazi fomu zote namba V11,” alisema Tendai Biti, ambaye ni kiongozi mwandamizi wa MDC.
Serikali kupitia waziri wa Mambo ya Ndani, Obert Mpofu imewataka wapinzani kujiepusha na utangazaji wa matokeo vinginevyo watafunguliwa mashtaka na kutupwa jela kwani ni kinyume cha sheria ya uchaguzi.
“Kama Serikali tumebaini vitendo vinavyofanywa na viongozi wa vyama vya siasa ambao kwa uwazi wametangaza matokeo kinyume cha sheria. Wakiendelea watachukuliwa hatua za kufunguliwa mashtaka na wanaweza kufungwa jela wakikutwa na hatia,” alisema Mpofu.
Hata hivyo, Rais Emmerson Mnangagwa pia amewaeleza wafuasi kuwa kutokana na ufuatiliaji uliofanywa na timu yake, kuna dalili nzuri ya ushindi.
“Habari za Asubuhi Zimbabwe. Nimefurahishwa na wingi wa watu waliojitokeza kupiga kura. Taarifa kutoka kwa wawakilishi wetu vituoni ziko chanya kupita kiasi! Tuendelee kuvumilia tukisubiri matokeo rasmi kwa mujibu wa Katiba,” Mnangagwa ameandika kupitia Twitter.
Tume ya uchaguzi imewataka wananchi na vyama vyote vya siasa kuwa wavumilivu wakati taratibu za kukusanya na kuhesabu kura zikiendelea. Hadi jana, ni matokeo ya majimbo saba tu kati ya 210 yaliyotangazwa ambapo Zanu-PF ilipata wabunge sita.
Tume hiyo kwa mujibu wa katiba itatangaza matokeo ya urais ndani ya kipindi cha siku tano.
Takribani 70% ya wapiga kura walijitokeza kupiga kura jana huku waangalizi wa kimataifa wakisubiriwa kutoa maoni yao.