Mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba watacheza na timu ya Asante Kotoko ya Ghana katika tamasha la klabu hiyo (Simba Day) ambalo hufanyika Agosti 08 kila mwaka.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Sunday Manara amethibitisha mchezo huo wa Agosti 08, katika mkutano na wandishi wa habari uliofanyika kwenye hoteli wa Serena jijini Dar es salaam.
Manara amesema kikosi chao kitachuana na timu hiyo kongwe ukanda wa Afrika Magharibi ambayo inashiriki Ligi Kuu Ghana, kwa kuamini itakua ni kipimo kizuri kwa vijana wao ambao kwa sasa wameweka kambi nchini Uturuki.
Manara amewatangaza Kotoko kucheza nao baada ya hapo awali kuenea kwa taarifa kuwa Simba imewaalika wapinzani wakubwa wa Gor Mahia FC, AFC Leopards kutoka Kenya lakini amezikanusha akisema hazikuwa na ukweli.
Kikosi hicho baada ya kambi yake kumalizika kitaanza safari ya kurejea nchini kuanzia tarehe 4 mwezi huu tayari kwa tamasha hilo kubwa linalofanyika kila mwaka.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Ghana, Kotoko wamecheza mechi 15 wakiwa kwenye nafasi ya 4 huku wakijikusanyia alama 24 na Ashanti Gold iliyo nafasi ya kwanza ina alama 27 ikiwa imecheza michezo 15 pia.