Zambia, Lusaka wamejitokeza kupinga vikali utekelezwaji wa tozo ya 30 Ngwe sawa na dola za Marekani 0.1 kwa watumiaji wa mitandao ya WhatsApp, Skype na Viber.
Uamuzi wa kutoza fedha kwa watumiaji wa mitandao hiyo ulipitishwa Jumatatu na Baraza la Mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Edgar Lungu.
Wanahabari wameambiwa kwamba viwango vipya vya tozo vimewekwa kulinda tasnia ya mawasiliano na ajira katika makampuni ya mawasiliano baada ya kuibuka wimbi kubwa la matumizi ya intaneti kwenye simu kwa gharama za watumiaji wa simu za kawaida.
“Ajira kama vile za wafanyakazi wa vibanda vya kupiga simu, wauzaji wa muda kwa mazungumzo, mafundi zitashuka ghafla ikiwa Wazambia watazidi kuhamia kwenye intaneti za simu na hivyo kujikuta wanaongeza ajira Marekani na kwingineko,” alisema waziri wa habari na msemaji wa serikali, Dora Siliya.
Serikali inadai kwamba asilimia 80 ya watu milioni nane ni watumiaji simu mara kwa mara wanapiga simu kwa kutumia Whatsapp, Viber na Skype.
Lakini Wazambia wakiwemo mabloga, wanasiasa wa upinzani na raia wa kawaida wametoa wito kuondolewa tozo hiyo mpya wakidai watumiaji hao hununua vifurushi kutoka kwenye kampuni za mawasiliano ili waweze kufanya mawasiliano.