Imeripotiwa kuwa meneja wa klabu ya Arsenal, Unai Emery ameingia katika vita na kiungo Mesut Ozil, hali ambayo ilipelekea kutomjumuisha kwenye kikosi kilichocheza mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya West Ham Utd.
Wawili hao wanadaiwa kuwa katika mvutano wa kiufundi, kufuatia kiwango duni kilichoonyeshwa na Ozil wakati wa mchezo wa mzunguuko wa pili wa ligi kuu ya England dhidi ya Chelsea, hali ambayo ilisababisha meneja Emery kumtoa kiungo huyo kipindi cha pili.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini England vimebaini kuwa maamuzi ya meneja huyo kutoka nchini Hispania ya kutompanga Ozil wakati wa mchezo dhidi ya West Ham Utd uliomalizika kwa ushindi wa mabao matatu kwa moja, yamemkera kiungo huyo kutoka nchini Ujerumani.
Ozil alikuwa na matumaini makubwa ya kucheza mchezo huo uliounguruma kwenye uwanja wa Emirates, lakini dakika za mwisho Emery alithihibitisha kumuacha nje ya kikosi baada ya kutoa orodha ya wachezaji waliopaswa kucheza dhidi ya Wagonga Nyundo.
Hata hivyo kabla ya kubainika kwa vita inayoendelea baina ya wawili hao, Emery alioulizwa kwa nini hakumjumuisha kikosini Ozil katika mchezo huo alisema, “siku mbili kabla ya mchezo huu nilizungumza naye kuhusu mambo kadhaa ya kiufundi ambayo nilipanga kuyatumia dhidi ya West Ham Utd kwa kumshirikisha kama mchezaji lakini cha kushangaza alinijibu hatoweza kucheza kwa sababu anaumwa.”
‘Siku ya Ijumaa baada ya mazoezi aliendelea kudai ni mgonjwa hivyo hatoweza kucheza dhidi ya West Ham Utd. Alizungumza na daktari na kumthibitishia suala hilo, na alishauriwa kupumzika nyumbani. Lakini cha kushangaza saa moja kabla ya mchezo alionekana katika chumba cha kubadilishia akiwa na wachezaji wenzake.’
Mpaka sasa Ozil hajazungumza lolote kuhusu kinachoendelea kati yake na meneja huyo aliyerithi mikoba kutoka kwa mzee Arsene Wenger, na haijulikani kama ataendelea kuwekwa nje ya kikosi kuelekea mchezo wa mzunguuko wa tatu dhidi ya Everton.