Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jimbo la Jiangsu nchini China katika sekta ya kilimo na viwanda utaiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020 na ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Majaliwa amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Gavana wa Jimbo la Jiangsu nchini China, Guo Yuan Qiung kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini China.
Amesema jimbo la Jiangsu ni miongoni mwa majimbo yaliyopiga hatua kubwa ya maendeleo kwenye teknolojia na viwanda duniani na Tanzania inahitaji wawekezaji wa uhakika katika sekta ya kilimo hususani watakaowekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, kuongeza thamani na kutafuta masoko.
“Tunathamini mchango wa Jimbo la Jiangsu katika uchumi wa Tanzania, ambapo sasa wawekezaji kutoka jimboni humo, waliowekeza kwenye viwanda mbalimbali kama cha kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na kukamua mafuta ya kula kwa kutumia mbegu za pamba cha Jielong kilichopo wilayani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha Urafiki cha jijini Dar es Salaam.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema bado mchango wa jimbo hilo unahitajika katika uendelezaji viwanda hususan katika masuala ya teknolojia ya viwanda, kuimarisha utafiti kwenye sekta ya kilimo na kuisaidia Tanzania kupata masoko ya mazao kama mbaazi, muhogo na soya. “Tunaomba uendelee kuhamasisha kampuni nyingi zaidi kutoka jimboni kwako kuja kuwekeza nchini.
Kuhusu kiwanda cha nguo cha Urafiki cha jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu na Naibu Gavana huyo walikubaliana kuangalia uwezekano wa kufanya mapitio ya changamoto za uendeshaji wa kiwanda hicho ili kutafuta suluhisho la mapungufu yanayojitokeza katika kiwanda hicho.