Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepiga marufuku Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutumia madalali kupangisha nyumba hizo na kuwadai kodi ya zaidi ya miezi sita.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa NHC mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema ni marufuku kwa baadhi ya watumishi wa shirika hilo kutumia vishoka na kulazimisha wananchi kulipa kodi ya nyumba kwa zaidi ya miezi sita.
Lukuvi alisema Serikali inakemea vikali na haitavumilia kuona tabia ya watumishi wa shirika hilo wakidai wananchi kodi ya zaidi ya miezi sita.
“Hii tabia Serikali tunaikemea na hatupendi kuona wananchi maskini wakinyanyasika katika nchi yao, Ningependa shirika la nyumba muonyeshe huduma ya mfano bora wa kupangisha na kudai kodi ya mwenzi mmoja tofauti na wapangishaji binafsi wanadai maskini kodi ya zaidi ya miezi sita,
Awali, Meneja wa NHC mkoani humo, Juma Kiaramba alisema kwa mwaka 2017/18 walifanikiwa kukusanya Sh2.8 bilioni sawa na asilimia 100.58.
“Kutokana na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa kodi zetu tumefanikiwa kukusanya Sh.2.82 bilioni mwaka wa fedha ulioisha Juni wa 2017/18, Tulifanya ukarabati wa majengo yetu kwa kutumia Sh255 milioni hadi sasa tunadai wapangaji wetu Sh54 milioni,” alisema Kiaramba.
Alisema shirika hilo litaanza kujenga nyumba 25 za gharama nafuu na tayari wametenga kiasi cha Sh1.4 bilioni ambapo itachukua miezi 18 kuanzia sasa.