Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza ametupilia mbali msamaha aliouomba Wema Sepetu baada ya video zake chafu kuonekana mtandaoni.
Shonza amesema kuwa utetezi na msamaha aliouomba msanii huyo hauna mashiko na kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vinavyohusika na Sanaa pamoja na udhibiti wa mawasiliano vitamuadhibu ipasavyo.
“Bodi ya Filamu imechukua hatua, lakini bado Mamlaka nyingine zitatekeleza majukumu yake katika hilo, asubiri adhabu ya TCRA,” Shonza amekaririwa.
Akizungumzia sentensi alizozitaja muigizaji huyo wakati anaomba radhi kupitia vyombo vya habari kuwa huenda ni utoto uliosababisha afanye kosa hilo, alisema hiyo sio sababu ya kweli bali hajitambui kwa nafasi aliyonayo kwenye jamii.
“Wema hana utoto wowote. Miaka 30 ukasema mtoto, mimi nina miaka 31 mbona sifanyi vitu kama hivyo na sijawahi kufanya?” Alihoji.
Bodi ya Filamu tayari imeshashusha rungu lake kwa Wema, likitangaza kumfungia kujihusisha na masuala ya filamu kwa kipindi kisichojulikana.
Kwa upande wa TCRA, bado hawajatoa tamko la adhabu yao, lakini kwakuwa Naibu Waziri ameeleza kuwa wako kwenye mchakato pia, ni dhahiri itakuwa inatokana na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii, Wema aliomba radhi na kueleza kuwa huahidi kuwa kitendo kama hicho kamwe hakitajirudia kwenye maisha yake.
Mashabiki wa msanii huyo pamoja na watu wengi maarufu walionesha kusikitishwa na kitendo cha Wema kurekodi kipande cha video kinachomuonesha akifanya yanayopaswa kufanya faragha, akiwa na mwanaume ambaye hivi karibuni alimtambulisha kuwa ndiye mumewe wa siku za usoni (future husband).