Israel imesema kuwa Iran inahusika na mashumbulizi ya makombora yaliyorushwa kwenye ardhi yake kutoka ukanda wa Gaza mwishoni mwa wiki.
Akizungumza jana kuhusu mashambulizi hayo yaliyoshuhudiwa tangu Ijumaa, msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Jonathan Conricus alidai kuwa yamefanywa na makundi yenye msimamo mkali kwa maelekezo na kusaidiwa na Iran.
Jeshi hilo limeeleza kuwa makombora 30 yalirushwa kwenye ardhi ya Israel na kwamba mfumo wao wa kijeshi ulifanikiwa kuzuia ziadi ya makombora 12.
Alisema kuwa makundi mawili yenye itikadi kali yanayosaidiwa kifedha na Iran, yalitekeleza mashambulizi hayo yakisaidiwa pia moja kwa moja na jeshi la Iran ambalo lina vikosi nchini Syria.
Aidha, Israel imetishia kuishambulia kijeshi Iran kwa kupiga vikosi vyake vilivyoko nchini Syria kama sehemu ya hatua za kulipa kisasi.
“Usiku wa jana tulipeleka ujumbe huu kwa pande husika, na ninasisitiza kuwa majibu yetu hayatakuwa na mipaka ya kijografia,” alisema Conricus.
Kwa mujibu wa CNN, mashambulizi ya Ijumaa yalianza kushuhudiwa majira ya jioni na kusababisha muonekano mwekundu kwenye eneo la ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israel limeeleza kuwa kwa majibu ya awali, ndege zake za kivita zilishambulia takribani maeneo 100 ya adui zao ikilenga maeneo ya kutengenezea silaha pamoja na vifaa vya kijeshi vinavyomilikiwa na makundi yenye itikadi kali pamoja na jeshi la Hamas ambalo linaidhibiti Gaza.