Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka watanzania kutolihusisha suala la kuwatafuta watekaji wa bilionea Mohammed Dewji na ubaguzi wa ufuatiliaji wa matukio hayo kati ya watu wa chini na wenye uwezo kifedha.
Akizungumza leo katika kituo kikuu cha polisi jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu kuhusu hatua iliyofikiwa na jeshi hilo katika kuwasaka watekaji wa Mo Dewji, Lugola alisema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa matukio yote na sio la Mo Dewji peke yake.
Aidha, alionesha kushangazwa na swali hilo linalomlenga Mo Dewji peke yake linalojirudia mara kwa mara bila kuhusisha watu wengine waliowahi kukumbwa na tukio kama hilo.
“Kwahiyo ninyi msidhani kwamba wale watu wenye hadhi ya chini kwamba hatuwatafuti. Kila mkituuliza mnaulizia Mo tu. Nawaomba waandishi wa habari tuwe waangalifu sana, mwisho mtaleta dhana katika nchi hii kwamba watu wa kawaida wanapopata matatizo hawana thamani, pengine hawatafutwi,” Waziri Lugola alisema.
“Serikali ya Magufuli ni serikali ambayo inamjali kuanzia yule mtu wa nchini mnyonge hadi yule tajiri wa mwisho. Anapopata tatizo lolote la kiusalama tunamjali kama tunavyomjali raia yeyote wa nchi hii,” aliongeza.
Mo Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Oktoba 11 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kuachiwa huru na watesi wake siku tisa baadaye walipomtelekeza katika eneo la Gymkhana jijini humo.
Mbali na Mo Dewji, wengine waliowahi kupotea katika mazingira yanayoripotiwa kuwa ni kutekwa ni pamoja na Ben Saanane ambaye ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, mwandishi wa habari wa gazeti la The Citizen/Mwananchi, Azory Gwanda, wasanii Roma Mkatoliki, Moni pamoja na mtayarishaji wa muziki maarufu kama Bin Laden; na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma Simon Kanguye.
Kati ya waliotajwa hapo juu ni wasanii Roma Mkatoliki, Moni na Bin Laden ndio waliachiwa huru na watekaji wao. Genge la watekaji bado linatafutwa.