Wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kyaani iliyoko Kitui nchini Kenya, jana usiku walifanikiwa kuwadhibiti wanafunzi wa kiume waliovamia bweni lao kwa lengo la kuwabaka.
Kwa mujibu wa Citizen, wasichana hao kwa msaada wa walinzi wa shule hiyo, waliwakamata na kuwakabidhi kwa Polisi wanafunzi hao wawili wenye umri wa miaka 18 wanaosoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya Kauma.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Kyaani, Elizabeth Musyimi, alipata taarifa kutoka kwa mlinzi wa shule hiyo majira ya saa sita kasoro robo usiku kuhusu uvamizi huo katika bweni la wasichana.
Wanafunzi hao wa kiume wanadaiwa kuingia katika eneo la shule hiyo kwa kukata nyaya za uzio wa shule na baadaye kuingia katika bweni lililotajwa kwa jina la ‘Upendo’ ambalo lina wanafunzi 47 wa kike.
Kwa mujibu wa kiongozi wa bweni hilo, wanaume hao wavamizi walianza kwa kurusha mawe kwenye paa ili kuzua taharuki kabla ya kuingia ndani.
“Hata hivyo, wanaume walioingia ndani ya bweni walikutana na nguvu ambayo hawakuitegemea. Kiongozi wa bweni alihamasisha morali kwa wenzake; na kwa msaada wa walinzi wa shule waliokuwa zamu waliwazidi nguvu wavamizi na kuwakamata,” Imeeleza taarifa ya Polisi.
Polisi wameeleza kuwa wanawashikilia watuhumiwa hao wakisubiri kuwafikisha mahakamani.