Nahodha na mshambuliaji wa klabu bingwa nchini Hispania Lionel Messi amejumuishwa kwenye safari ya kuelekea Italia, kwa ajili ya mchezo wa mkondo wanne wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi dhidi ya Inter Milan.
Messi amejumuishwa kikosini, baada ya kuwa majeruhi kwa muda wa majuma mawili, kufuatia kuteuka mkono akiwa katika mchezo wa ligi kuu ya Hispania dhidi ya Sevilla, uliomalizika kwa FC Barcelona kupata ushindi wa mabao manne kwa mawili.
Hatua ya jina la mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina kuingia kwenye msafara wa Italia, imewashtua wengi klabuni hapo kutokana na taarifa za awali kueleza kwamba, huenda Lionel Messi angekuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya majuma matatu.
Tarifa iliyothibitisha kusafiri kwa Messi ilieleza kuwa “Mchezaji huyu atasafiri na tayari jopo la madaktari limeshajiridhisha, anaweza kuwa sehemu ya kikosi kitakachopambana dhidi ya Inter Milan keshokutwa jumatano”.
Messi alikosa mchezo wa mkondo wa tatu wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Inter Milan uliomalizika kwa FC Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri, kisha akaendelea kuwa nje ya kikosi kwenye mchezo wa ligi ya Hispania uliowakutanisha na Real Madrid waliokubali bakora 5 kwa 1.
Messi alirejea mazoezini juma lililopita, lakini hakucheza mchezo wa jumamosi dhidi ya Rayo Vallecano ambao walifungwa mabao matatu kwa mawili.
FC Barcelona wanaongoza msimamo wa kundi B, baada ya kushinda michezo mitatu, huku wapinzani wao Inter Milan wakishika nafasi ya pili kwa kushinda michezo miwiwli na kupoteza mmoja.