Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara ambaye ni mteule wa nafasi ya Unaibu Waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ametoa kauli yake ya kwanza tangu apate uteule huo akitoa onyo kali kwa watakaotaka kumkwamisha.
Waitara amesema kuwa yuko tayari kushirikiana na kila mtu katika utendaji wake wa kazi, lakini hatakubali kukwamishwa na mtu yeyote bila kujali itikadi yake ya kisiasa.
“Awe mpinzani au mtu yeyote, sitakubali anikwamishe. Ninaahidi kushirikiana na mtu yeyote. Ninamshukuru Mungu kwa nafasi hii na naahidi kuitumikia kwa moyo wangu wote,” Waitara aliiambia Mwananchi.
Aidha, Waitara ameeleza kuwa hakufahamu kama atapata uteuzi huo kwani hakujua kama Rais John Magufuli angefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la Mawaziri.
Waitara atakuwa miongoni mwa wateule wapya wa baraza la mawaziri watakaoapishwa leo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tayari kwa kuanza kazi.
Mwanasiasa huyo alijiuzulu ubunge na kuhama Chadema, kisha kuhamia CCM ambapo aligombea na kurejea tena kwenye nafasi yake ya Ubunge wa Ukonga.